Jumapili , 22nd Oct , 2017

Jeshi la Polisi mkoani Singida linatarajia kumfikisha Mahakamani Minga Daud Idd ambaye ni mganga wa kienyeji mkazi wa mtaa wa Minga kwa tuhuma ya kunajisi watoto 14.

Kaimu kamanda wa Polisi mkoa wa Singida Isaya Mbughi amethibitisha hilo ambapo amesema upelelezi unaendelea na muda wowote kuanzia kesho mtuhumiwa huyo Daud Idd mwenye miaka 74 atafikishwa mahakamani.

“Ni kweli tunamshikilia Daudi Idd kwa tuhuma ya kunajisi watoto 14 wenye umri kati ya miaka saba na 12 na kuwasababishia maumivu makali katika sehemu zao za siri, na upelelezi unaendelea ambapo muda wowote kuanzia kesho atafikishwa mahakamani”, amesema Kamanda Mbughi.

Kamanda amesema walibaini vitendo hivyo Oktoba 16 baada ya mtoto mmoja mwenye umri wa miaka saba kulalamika kuwa anasikia maumivu sehemu za siri akiwa anaogeshwa na Mama yake, ndipo Mama yake akafuatilia na mtoto kueleza kuwa vitendo hivyo hufanyiwa yeye na wenzake.

Baada ya Mama huyo kuambiwa na mwanae kuwa Mzee Daud maarufu Babu Karatu ndio anawafanyia vitendo hivyo Mama aliripoti kwa mwenyekiti wa mtaa wa Minga kisha wakaripoti Polisi ndio hatua za kumkamata mganga huyo wa kienyeji zikafuata.