Ijumaa , 17th Mar , 2017

Rais John Magufuli amemuagiza DC Bagamoyo kuwasaka, kuwakamata na kuwafikisha katika vyombo vya sheria wafugaji wote wanaodaiwa kuhusika katika matukio ya kuwashambulia kwa viboko wananchi wa Kijiji cha Fukayosi kilichopo Wilayani humo.

Rais Magufuli akisiliza changamoto za wakulima na wafugaji katika kjijiji cha Fukayosi wilaya ya Bagamoyo mkoa wa Pwani aliposimama kwa muda.

Mhe. Dkt. Magufuli aliyekuwa akisafiri kwa gari kutoka Dodoma kwenda Jijini Dar es Salaam ametoa agizo hilo leo tarehe 17 Machi, 2017 aliposimama katika kijiji hicho baada ya kuona wananchi wengi wakiwa wamekusanyika kando ya Ofisi ya Kata.

Baada ya kusimamisha msafara wake, Mhe. Rais Magufuli aliwaita wananchi waliokuwa wamekusanyika huku wakiwa wameshika mabango yaliyoandikwa ujumbe wa kutaka wafugaji wa jamii ya Wamang’ati waondolewe na kisha akatoa nafasi kwa baadhi yao kueleza dukuduku lao.

Wananchi hao ambao ni wakulima na mfugaji mmoja aliyejitokeza wakaeleza kuwa Wamang’ati wamekuwa wakiwanyanyasa kwa kuingiza mifugo katika mashamba yao ya mazao na wakithubutu kuwakataza wamekuwa wakichapwa viboko na baadhi kuuawa.

Magufuli akitoa maagizo kwa Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo Mhe. Maggid Mwanga baada ya kuongea na wanakjijiji wa  Fukayosi wilayani humo aliposimama  kwa muda 

Katika majibu yake, pamoja na kutaka wote wanaodaiwa kuwashambulia wananchi kwa viboko wakamatwe Mhe. Rais Magufuli amemtaka Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Alhaji Majid Mwanga kukomesha mara moja vitendo vya wafugaji kuwapiga wakulima na wakulima kuwapiga wafugaji, na pia kukomesha vitendo vya wafugaji kulisha mifugo yao katika mashamba ya wakulima.

“Kuanzia leo isitokee mfugaji kumpiga mkulima, mkulima kumpiga mfugaji wala mfugaji kulisha mifugo yake kwenye mashamba ya wakulima, na suala hili nitalifuatilia mimi mwenyewe.

“Kwa hiyo Mkuu wa Wilaya na Viongozi mlishughulikie hili kabla mimi sijawashughulikia nyinyi, wale waliopiga watu, nataka wote wakamatwe na wafikishwe kwenye vyombo vya sheria” amesema Mhe. Dkt. Magufuli.

Magufuli akiongea na wanakjijiji wa  Fukayosi wilaya ya Bagamoyo mkoa wa Pwani