Jumanne , 27th Sep , 2016

Rais Magufuli ametengua uteuzi wa Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera Bw. Amantius Msole na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba Bw. Steven Makonda.

Rais Magufuli

Rais Magufuli amefanya maamuzi hayo baada ya kubaini kuwa wamefungua akaunti nyingine ya benki kwa kutumia jina linalofanana na akaunti rasmi ya kuchangia maafa iitwayo "Kamati Maafa Kagera" kwa lengo la kujipatia fedha.

Taarifa iliyotolewa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa muda mfupi baada ya kupokea hundi ya msaada kutoka kwa Waziri Mkuu wa India imeeleza kuwa pamoja na kutengua uteuzi huo Rais Magufuli ameagiza vyombo vya dola vichukue hatua dhidi ya wote waliohusika katika njama za kufungua akaunti hiyo.

Aidha, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa amemsimamisha kazi Mhasibu Mkuu wa Mkoa wa Kagera Bw. Simbaufoo Swai kutokana na kuhusika katika njama hizo.

Hata hivyo Mhe. Kassim Majaliwa ametoa wito kwa wananchi na taasisi mbalimbali kuendelea kuchangia misaada kwa ajili ya walioathirika kwa kutumia akaunti rasmi ya "Kamati Maafa Kagera" ambayo imetangazwa na Serikali.