Ijumaa , 3rd Jun , 2016

Madhara ya zoezi la uzimaji wa simu bandia litakalofanywa na Mamlaka ya Mawasiliano TCRA ifikapo Juni 16 mwaka huu yameanza kuonekana kwa wafanyabiashara wa simu eneo la Kariakoo ambao baadhi yao wamefilisika na kuanza kufunga biashara zao.

Wakizungumza na EATV iliyotembelea eneo hilo hii leo, wafanyabiashara hao wamesema kadri siku zinavyozidi kwenda wateja wamekuwa wakipungua kwa kasi huku wengi wakiacha kununua simu hadi lipite zoezi hilo wakiamini kwamba simu zitakazokwepo baada ya muda huo ndio zitakuwa simu halisi.

"Hili zoezi kwa kweli limesababisha baadhi yetu tufilisike kabisa...kama mimi hapa sina cha kuuza nimekula mtaji baada ya wateja kutofika dukani kwangu na sasa sina cha kuuza nimeamua kufunga duka nijaribu kufanya kitu kingine," amesema mmoja wa wafanyabiashara hao.

Wakiwa na nyuso zilizokata tamaa, wafanyabiashara hao wamesema kinachowaumiza sana ni mikopo waliyokopa kutoka taasisi za fedha ambayo wanatakiwa kuilipa kwa mujibu wa makubaliano waliyoingia na mabenki na taasisi husika za kifedha.

Aidha, katika kile walichokieleza kuwa ni madhara ya kisaikolojia; wafanyabiashara hao wameitaka TCRA kutobadilisha tarehe ya utekelezwaji wa zoezi hilo ili kurejesha imani kwa wateja kwani licha ya biashara ya simu, uchangamfu wa biashara katika eneo zima la Kariakoo hivi sasa umepungua.

"Kwa jinsi hali ilivyo sasa tunatamani hilo zoezi la kusima simu bandia litekelezwe haraka sana kwani tumekuwa tukiathirika kisaikolojia kwani kwa upande mmoja unaambiwa simu unazouza ni feki wakati sio kweli lakini wakati huo huo hata hizo simu halisi unazouza wateja wanaogopa kununua...sasa ni bora mbivu na mbichi zijulikane mapema," amesema mfanyabiashara Andrew Mashauri.