Jumatatu , 20th Mar , 2017

Chama cha Madaktari nchini, MAT, kimepinga mpango wa kuwatuma madaktari 500 nchini Kenya wakisema Tanzania ina upungufu mkubwa wa madaktari.

Rais Magufuli akiwa katika mazungumzo na Waziri wa Afya kutoka nchini Kenya Dkt. Cleopa Mailu kuhusu Tanzania kupeleka madaktari 500 nchini Kenya, Ajira za Madaktari hao zitatangazwa mara moja na Waziri wa Afya Ummy Mwalimu na zitawahusu Madaktari ambao hawajaajiriwa Serikalini(hawapo katika utumishi wa umma au taasisi za serikali) waliomaliza mafunzo kwa vitendo na ambao wamesajiliwa na Baraza la Madaktari la Tanganyika.

Pingamizi hilo linafuatia makubaliano kati ya serikali ya Tanzania na Kenya mwishoni mwa wiki iliyopita ambapo Tanzania ilikubali kutuma madaktari wapatao 500 nchini Kenya.

Pamoja na masuala mengine, maafisa wa chama cha MAT wamesema, wanahitaji ufafanuzi kuhusu ni kwa nini Serikali ya Kenya imeshindwa kuajiri Madaktari wake na kuanza kutafuta Madaktari kutoka Tanzania huku ikizingatiwa kwamba malipo ya Madaktari wa Tanzania yatakuwa makubwa zaidi ya wenyeji.

Kadhalika taarifa iliyotolewa na MAT imehoji ni kwa nini suala hili linafanyika wakati Kenya ikielekea kwenye Uchaguzi Mkuu, na kuhoji pia nani atawajibika katika suala la usalama wa Watanzania hasa ikizingatiwa kwamba tayari kuna viashiria vya chuki, na ikizingatia Kenya bado ina changamoto za kiusalama.

Madaktari katika mafunzo

MAT imesisitiza kwamba ni muhimu kusitisha zoezi la kuwapeleka Madaktari wa Tanzania mpaka hapo Serikali ya Kenya itakapoanza utekelezaji wa makubaliano kati yake na Madaktari wao,

Kenya imeshuhudia mgomo wa madaktari uliomalizika wiki iliyopita baada ya kudumu kwa siku 100.