Madaktari 209 kutupwa TAMISEMI

Thursday , 20th Apr , 2017

Serikali imeagiza Madaktari 209 kati ya Madaktari 258, watakaoajiriwa na Serikali kwa agizo la Rais Dk. John Pombe Magufuli, wapelekwe Ofisi ya Rais Tamisemi ili kwenda kuongeza nguvu kazi na kukabili uhaba wa madaktari maeneo ya vijijini.

Waziri Ummy Mwalimu

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, ametoa agizo hilo leo Jijini Dar es Salaam kwenye mkutano na wataalamu na madaktari bingwa wa masuala ya wanawake na uzazi kutoka ndani na nje ya nchi ambapo amesema maeneo ya vijijini bado yana changamoto kubwa sana ya kukosa madaktari bingwa hasa wa masuala ya kina mama wajawazito.

Amesema, moja ya changamoto ni 64% tu ya wanawake ndio wanajifungulia eneo lenye mhudumu wa afya na kwamba, tayari maelekezo yametolewa kwa Wakurugenzi wa halmashauri nchini kuhakikisha wanaboresha mazingira ya wajawazito.

Kwa upande wake Rais wa AGOTA Andrea Pembe amesema katika takwimu walizonazo kwa sasa kila watoto laki moja wanaozaliwa hai wanafariki kutokana na swala la uzazi usio na mpango na kuwataka kina mama kuzingatia maelekezo ya wataalamu wa afya kuhusu huduma muhimu na kuiomba serikali iboreshe huduma za afya ya uzazi.