Jumatatu , 16th Jan , 2017

Utafiti uliofanywa na shirika la Oxfam la Uingereza unaonesha mabilionea wanane wanamiliki mali sawa na mali ya watu 3.6 bilioni duniani kwa pamoja.

Bill Gates

Takwimu za shirika hilo, ambazo zimepingwa na baadhi ya wakosoaji, zinatokana na maelezo na habari za kina zilizokusanywa na shirika hilo, na zinaonesha pengo kati ya matajiri na maskini ni kubwa "kuliko ilivyodhaniwa awali".

Ripoti hiyo ya Oxfam imetolewa wakati mkutano mkubwa kuhusu uchumi wa dunia unaanza mjini Davos nchini Uswisi.

Mark Littlewood, wa Taasisi ya Masuala ya Uchumi, amesema Oxfam inapaswa kuangazia njia ya kusisimua ukuaji wa uchumi   wa dunia badala ya kufanya utafiti huo.

Oxfam imekuwa ikitoa ripoti zinazokaribiana kwa miaka minne iliyopita ambapo mwaka 2016 ilifichua kwamba watu 62 duniani walikuwa na utajiri sawa na wa nusu ya watu maskini zaidi duniani.

Lakini bado hali ni ile ile, kwamba asilimia moja ya watu duniani wanamiliki utajiri sawa na watu hao wengine wote duniani kwa pamoja.

Amancio Ortega

 

Mabilionea wanane matajiri zaidi duniani ni

1. Bill Gates (US): mwanzilishi wa Microsoft (utajiri wake $75bn)

2. Amancio Ortega (Spain): mwanzilishi wa Zara na mmiliki wa Inditex (utajiri wake $67bn)

3. Warren Buffett (US): mwenyehisa mkubwa Berkshire Hathaway (utajiri wake $60.8bn)

4. Carlos Slim Helu (Mexico): mmiliki wa Grupo Carso (utajiri wake $50bn)

5. Jeff Bezos (US): mwanzilishi na afisa mkuu mtendaji wa Amazon (utajiri wake $45.2bn)

6. Mark Zuckerberg (US): mwanzilishi mwenza na afisa mkuu mtendaji wa Facebook (utajiri wake $44.6bn)

7. Larry Ellison (US): mwanzilishi mwenza na afisa mkuu mtendaji wa Oracle (utajiri wake $43.6bn)

8. Michael Bloomberg (US): mmiliki wa Bloomberg LP (utajiri wake $40bn)

Warren Buffett

Chanzo: Orodha ya mabilionea ya Forbes, Machi 2016