Jumatatu , 28th Sep , 2020

Mgombea Urais kupitia,Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, amesema kuwa hajapokea malalamiko yoyote kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), yanayohusu mwenendo wa ufanyaji wa kampeni zake, huku akidai kuwa hatohudhuria suala lolote linalohusiana na kampeni zake.

Mgombea Urais kupitia CHADEMA Tundu Lissu.

Lissu ametoa kauli hiyo kupitia ukurasa wake wa mtandao wa Twitter, yakiwa yamepita masaa kadhaa tu tangu NEC, ilipotoa tamko la kwamba, imemuandikia barua mgombea huyo kwa tuhuma mbalimbali ikiwemo kuikashifu NEC kwamba itaiba kura zake, pamoja na madai ya kwamba mgombea urais wa CCM, Dkt. Magufuli atakutana na wakurugenzi wa Halmashauri hivi karibuni.

"Sijapokea malalamiko yoyote juu ya jambo lolote linalohusiana na kampeni za uchaguzi mkuu huu kutoka NEC, sijapokea wito wowote kuhusu jambo lolote linalohusiana na kampeni za uchaguzi mkuu huu kutoka NEC, sitarajii kuacha kampeni ili kuitikia wito wa mitandaoni wa mtu yeyote", ameandika Lissu.

Jana Septemba 27, 2020, Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi (NEC) Dkt. Charles Mahera, wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari mkoani Arusha, alisema kuwa Lissu alitoa tuhuma hizo kwenye mikutano yake ya kampeni mjini Musoma kati ya Septemba 25 na 26 mwaka huu.