Lipumba na Maalim Seif watafute maridhiano - ADC

Sunday , 16th Jul , 2017

Chama cha Alliance for Democratic Change ADC kimewaomba viongozi wanaopingana ndani ya Chama cha Upinzani - CUF, Profesa Ibrahim Lipumba na mwenzake Maalim Seif Sharif Hamad, kuketi kwenye meza ya mazungumzo na kumaliza mgogoro unaoendelea CUF.

Akizungumza na wanahabari katika ofisi kuu za chama hicho Buguruni jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa ADC Bw. Doyo Hassan Doyo amesema mgogoro huo umekuwa ukidhoofisha afya ya vyama vya upinzani huku akiitaka serikali hususani jeshi la polisi, kuchukua hatua dhidi ya vyama vingine vya siasa vinavyotoa matamshi yenye nia ya kuendeleza mgogoro huo alioutaja kuwa ni hatari kwa amani na usalama wa nchi.

Aidha, Doyo amesema ADC inalaani mauaji ya kuvizia yanayoendelea katika wilaya za Mkuranga, Kibiti na Rufiji mkoani Pwani na kwamba mauaji hayo hayakiathiri Chama Cha Mapinduzi peke yake bali hata vyama vingine ambavyo wafuasi na wanachama wake nao wameanza kuingia hofu ya kuwania nafasi mbali mbali za uongozi.