Jumatatu , 19th Oct , 2015

Tume ya Taifa ya Uchaguzi nchini NEC imetakiwa kubandika haraka majina ya wapiga kura vituoni ili wapiga kura wahakiki majina yao mapema kabla ya siku ya uchaguzi.

Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu LHRC Dr. Hellen Kijo-bisimba

Rai hiyo imetolewa na mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu LHRC Dr. Hellen Kijo-Bisimba wakati akiongea na East Africa Radio na kusisitiza kuwa kama tume ya uchaguzi wakichelewa kutoa majina hayo na baadaye watu wakakosa kuyaona siku ya kupiga kura na kuikosa haki yao ya msingi wanaweza kuzusha malalamiko na hata kupelekea machafuko na Vurugu.

Dr Kijo Bisimba ameongeza kuwa bado kuna tatizo sugu la kampeni za matusi, lugha za kejeli na kashfa dhidi ya wagombea wengine hata kuwatumia wasanii kuwakejeli na kuwatukana wagombea wengine.

Aidha Dr Bisimba amesema kuwa wagombea wanawake hawajawezeshwa vya kutosha na vyama vyao na hivyo wagombea wanawake kushindwa kufanya kampeni vizuri na kushindwa kuwafikia wapiga kura.