Jumamosi , 23rd Sep , 2017

Baada ya Rais Magufuli kuhutubia Arusha katika shughuli za kuwatunukia Kamisheni Maafisa ya Jeshi la Wananchi JWTZ na kisha kuwapa nafasi Madiwani kumi waliohama Chadema kwa madai ya kumuunga Rais mkono Wabunge wa Arusha wametaka kukutana na Rais

ili wamuoneyeshe rushwa ilivyotumika na watumishi wake.

Kupitia ujumbe wa Video uliowekwa na viongozi hao mtandaoni, Godbless Lema wa Arusha Mjini  pamoja na Joshua Nassari wa Arumeru Mashariki wamemtaka Rais Magufuli kuwapatia nafasi za kuweza kumthibitishia jinsi viongozi wake walivyoweza kutumia rushwa na kuwashawishi madiwani hao wa Chadema kuachia ngazi na kumhakikishia kuwa ushahidi wote wanao hivyo wao wapo tayari kumuonyesha hata mbele ya vyombo vya usalama.

Mh. Lema amesema kuwa wao kama Chadema hawana shida kwa viongozi hao kuondoka ndani ya chama chao na hata kama wataondoka wote, lakini wanachosikitika ni jinsi viongozi hao walivyofanya vitendo vya aibu na vya kumdhalilisha Mh. Rais kwa kutumia rushwa.

"Tuna taarifa tulizipata kwamba leo madiwani wawili wa Arusha mjini wangeondoka na kujiunga na CCM lakini kwetu siyo shida, Mh. Rais anapaswa kufahamu kwamba hakuna chochote kitakachofanyika kwenye ofisi za Mkuu wa mkoa, Mkuu wa Wilaya au Mkurugenzi ndani ya Arusha na sisi tusikipate. Sasa Mh. Rais. Mimi nataka umuite Nasarri, RPC, IGP na hata Takukuru tukupatie ushahidi. Mimim sitaweza kuja maana najua sipendwi sana.

Ameongeza kwamba "Tulikuwa tunasubiri tukio la leo, wewe ni Rais mcha Mungu na Kiongozi unayepinga Rushwa, hawa watu wanaosema wamejiunga na Chama chao utajua wamejiunga kwa sababu ya kukuunga mkono au wameunga rushwa na fedha mkono.  Hawa watu walioandaa hafla Mh. Rais wamekutia aibu sana na tutoe angalizo kwamba ushahidi huu haupo nyumbani kwetu msije kutufata upo hewani na mkituletea shida tutawaambia vijana wabonyeze Button ili usambae au pia usikutana na Nassari tutauachia.

Kwa Upande wa Mbunge Joshua Nassari amesema kesho watafanya mkutano na wanahabari na kuelezea rushwa ilivyotumika na viongozi kumdanganya Rais wa nchi na kusisitiza ushahidi wao hauna mashaka.