Jumatatu , 21st Aug , 2017

Mbunge wa Arusha Mjini Godbless Jonathan Lema amewageukia viongozi wa dini nchini kwa kusema kwamba wanapaswa kukemea vitendo vya udhalilishwaji wanavyofanyiwa wabunge wa upinzani na siyo kukemea viroba na bia.

Mbunge Godbless Lema

Lema aliitoa kauli hiyo wakati akizungumza na wanahabari Mjini Arusha na kusema kuwa viongozi wa dini mbalimbali nchini wasifumbe macho yao na kujifanya hawayaoni mateso wanayopatiwa viongozi wa upinzani nchini.

"Viongozi wetu wa dini wasijifanye hili tunalofanyiwa upinzani hawayaoni. Kazi ya viongozi wa dini siyo kukemea bia na viroba bali wanatakiwa wapige kelele kwenye ukiukwaji wa misingi ya sheria inayoendelea hapa nchini dhidi ya upinzani", alisema Lema.

Pamoja na hayo, Mhe. Lema ameongeza kuwa viongozi wa dini endapo watasimama katika kukemea maovu yanayofanywa ndani ya nchi yakiwepo ya unyanyasaji watakuwa wamelikomboa taifa kwenye machafuko.

"Ipo siku  kuna watu watashindwa kuvumiliwa haya tunayofanyiwa, hapo ndipo vita vya wenyewe kwa wenyewe vitakapokuja hapo siku za mbeleni" alimaliza.