Jumatatu , 25th Sep , 2017

Mbunge wa Singida Kaskazini Lazaro Nyalandu amesema kitendo cha Tundu Lissu kusalimika kifo kwenye tukio la kupigwa risasi ni Mungu tu ndiye aliandika, lakini kinamuumiza zaidi huku akilaumu ameikosea nini nchi mpaka kufanyiwa hivyo.

Lazaro Nyalandu ameyasema hayo kwenye ukurasa wake wa facebook, akiwa mkoani Mbeya ambapo alishiriki maombezi ya Tundu Lissu ambayo yalifanyika siku ya jana. 

"Nimekuja Mbeya kulikumbusha Taifa kuwa kupigwa kwa mmoja wetu ni kupigwa kwetu sote, kuumizwa kwake ni kuumizwa kwetu sote, na kudhulumiwa kwake huyo mmoja ni dhuluma dhidi ya kila Mtanzania. Tundu Lissu amepona kwa kuwa imeandikwa, naamini, ndani ya moyo wake akiwa katika maumivu lukuki aliyonayo, atakuwa anajiuliza nimekukosea nini Tanzania", ameandika Lazaro Nyalandu

Lazaro Nyalandu amekuwa miongoni mwa watu wanaofuatilia kwa karibu matibabu ya Tundu Lissu jijini Nairobi, huku akiimiza watanzania kuendelea kumuombea ili aweze kupona kabisa na kurejea kwenye hali yake ya kawaida.