Ijumaa , 17th Nov , 2017

Waziri wa Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu Jenista Joakim Mhagama amesema kuwa mapinduzi yoyote ya viwanda huanza na viwanda vidogo hivyo watu wasibeze dhana ya viwanda nchini.

Mh. Mhagama ameyasema hayo mjini Dodoma wakati akichangia mada kwenye kongamano la pili la kitaaluma la kuwasilisha matokeo ya tafiti juu ya mchango wa viwanda katika ukuaji wa uchumi endelevu.

“Maendeleo ya viwanda Tanzania kama ilivyo nchi nyingine yanatokana na kuwekeza nguvu katika viwanda vidogo, vya kati na hatimaye viwanda vikubwa na hakuna mapinduzi yoyote katika nchi kubwa yaliyoanza na viwanda vikubwa”.

Aidha waziri Mhagama ameongeza kuwa wapo watu wanaobeza viwanda vidogo na dhana nzima ya viwanda nchini ambapo amesema huo ni mtazamo finyu na umepitwa na wakati.

Waziri amewaomba wananchi kuunga mkono sera ya viwanda kwa kuanza na viwanda vidogo kisha viwanda vya kati na hatimaye lengo la kuwa na viwanda vikubwa litatimia kupitia kuanza na viwanda vidogo.