Ijumaa , 17th Nov , 2017

Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mh. Charles Mwijage amesema wafanyakazi wa kiwanda cha nguo cha Urafiki waliobinafsisha kiwanda hicho na kuiingizia hasara serikali watashughulikiwa ipasavyo.

Mwijage ameyasema hayo bungeni leo wakati akijibu maswali mawili ya nyongeza yaliyoulizwa na mbunge wa Ubungo Mh. Said Kubenea aliyetaka kujua hatua watakazo chukuliwa wafanyakazi walioshiriki kubinafsisha kiwanda cha urafiki kwa mwekezi kutoka China ambaye ameshindwa kuleta faida.

“Ukiiona ripoti ya mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali CAG utalia Kubenea, kwahiyo kila mtu aliyehusika kutuingiza kwenye dhahama hii rungu litamshukia kama Mwewe”, amesema Waziri Mwijage

.

Aidha Waziri amesema kuwa tayari serikali ipo mbioni kumaliza makubaliano na mwekezaji mpya kutoka China ambapo kiwanda hicho kitajengwa upya vizuri na serikali itanufaika kwa takribani asilimia 75.

Waziri Mwijage ameongeza kuwa kiwanda cha Urefiki ni cha kihistoria hivyo watakijenga upya na kitakuwa na wafanyakazi zaidi ya elfu nane.