Jumatano , 3rd Mar , 2021

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga, ametoa ushuhuda wa binti aliyekuwa akibakwa na bosi wake kwa mwaka mzima kwa lengo la kulinda ajira yake lakini walipotaka kumsaidia alikimbia kwa kuhofia kupoteza kazi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) Anna Henga

Kauli hiyo ameitoa hii leo Machi 3, 2021, kwenye kipindi cha Supa Breakfast cha East Africa Radio, wakati akizungumzia ukubwa wa tatizo la rushwa ya ngono makazini na hata mashuleni, na kusema kuwa tatizo la rushwa ya ngono lipo na mara nyingi wahanga wa tatizo hilo huwa hawatoi taarifa.

"Kuna msichana alikuwa anabakwa na bosi wake karibia mwaka mzima ili aweze kubaki kazini na wasichana wengi katika hiyo ofisi walikuwa wamefukuzwa kwa sababu wamemkataa bosi na yeye kwa vile alikuwa na shida akamvumilia na tulipotaka kumsaidia akakimbia kwa kuhofia kukosa kazi na hii rushwa ya ngono inawapata watu ambao hawana chaguo," amesema Anna Henga.

Aidha, Anna Henga, ameongeza kuwa, "Mwarobaini wa tatizo la rushwa ya ngono siyo mmoja inahitaji sekta mbalimbali kushirikiana ili kuliondoa maana ni mbaya sana na linadhalilisha utu".