Ijumaa , 15th Sep , 2017

Kijana wa kiume mwenye umri wa miaka 17 ambaye ana ulemavu wa ngozi amekutwa akiwa ameuawa na ubongo wake kutolewa  huko nchini Msumbiji.

Mkazi wa eneo la Tete, Magharibi mwa Msumbiji, ambaye hakutaka jina lake kutajwa, amesema wazazi wa mvulana huyo walianza kumtafuta alipokosa kurejea nyumbani.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Uingereza (BBC) zinasema kuwa mwili wa kijana huyo ulipatikana ukiwa hauna mikono na miguu huku  kichwa chake kikiwa kimepasuliwa na ubongo wake kutolewa.

Msemaji wa polisi wa mkoa wa Tete Lurdes Ferreira amesema polisi wataanzisha uchunguzi eneo ambalo uhalifu huo ulitokea.

Tukio hilo ndilo tukio la karibuni zaidi dhidi ya watu wenye ulemavu wa ngozi ambao mara kwa mara hushambuliwa kwa sababu ya ushirikina huku wakidai kuwa viungo vyao vinaweza kuleta utajiri.