Jumapili , 13th Aug , 2017

Naibu waziri wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Khamis Kigwangala, ameweka wazi sababu ya vijana wengi kufeli kwenye maisha na kusema kuwa wanapenda kuishi maisha yasiyo na uhalisia.

Kwenye ukurasa wake wa twitter ambapo alikuwa akijibizana na baadhi ya watanzania wanaotumia mtandao huo kuhusu tabia ya vijana kutopenda kujishughulisha na kuchagua kazi, Dkt. Kigwangala amesema vijana wa sasa hivi wengi wanapenda kuishi maisha ya kwenye mitandao, na kuacha yale yenye uhalisia na kuweza kujishughulisha kujikwamua kiuchumi, huku akiweka wazi malipo pekee sio sababu ya vijana wengi kuchagua kazi.

"Siyo malipo pekee, pia matarjio na matumizi ya vijana, wengi wanataka kuishi maisha ya 'Instagram' na 'Facebook'...badala ya uhalisia, tamaa ya maisha mazuri bila kupiga kazi nalo ni tatizo jingine, kubwa tu!", aliandika Dkt. Kigwangala.

Naibu Waziri Kigwangala aliendelea na mazungumzo hayo na kusema kuwa kwa jinsi hali ilivyo, kuna haja ya kuweka nguvu yenye ukali ili kuweza kutatua hali hiyo, na kushawishi vijana wajitambue kuishi maisha yenye uhalisia.

"Kama mapambano ni makali zaidi sasa tunapaswa tuandae nguvu na mbinu kali za kiwango cha ukali uliopo, siyo kukata tamaa, Na huo ndiyo mwanzo wa tofauti ya waliofanikiwa na wasofanikiwa, kusimama kwenye uhalisia ama kuleta ubishoo kwenye kazi", aliandika Dkt. Kigwangala.

Soma hapa mfululizo wa tweet zake