Ijumaa , 30th Sep , 2022

Mahakama ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, imetupilia mbali maombi ya wananchi wa jamii ya wafugaji ya Maasai katika kesi iliyohusisha mgogoro wa ardhi baina ya serikali ya Tanzania na wananchi hao wa wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha, baada ya wafugaji hao kushindwa kuthibitisha madai yao.

Wafugaji wa Kimaasai

Mahakama ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, imetupilia mbali maombi ya wananchi wa jamii ya wafugaji ya Maasai katika kesi iliyohusisha mgogoro wa ardhi baina ya serikali ya Tanzania na wananchi hao wa Ngorongoro mkoani Arusha, baada ya kushindwa kuthibitisha madai yao.

Akisoma maamuzi hayo ya mahakama JajI Charles Nyachae kwa niaba ya Jaji Monica Mugenyi, amesema kuwa waleta maombi ambao ni wafugaji wa jamii ya kimaasai walishindwa kuthibitisha madai yao ya kwamba waliteswa na kupigwa pamoja na kuharibiwa mali zao na watu waliowataja kuwa ni askari wa jeshi la polisi la Tanzania wakati wakiwaondoa kwenye makazi yao. 

Katika utetezi wao Mwanasheria Mkuu wa serikali ya Tanzania amebainisha kwamba, waliwaondoa wafugaji waliovamia Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, ambayo inapakana na eneo la Ngorongoro upande wa Kaskazini, na sio kweli kwamba waliwaondoa katika maeneo ya vijiji vyao kwa nguvu na kwa kuwatesa. 

Maelezo ya waleta maombi yaliyosomwa mahakamani hapo yanasema  kuwa miongoni mwa mashahidi walieleza jinsi walivyoshuhudia wananchi wakipigwa na watu wanaoaminika kuwa maafisa wa jeshi la polisi la Tanzania, na walishuhudia magari yaliyobeba askari wa polisi na pia waliwashuhudia maafisa wakiharibu nyumba, mifugo na mali zingine za wakazi hao. 

Baadhi ya Mawakili wa upande wa wapeleka mashtaka  na wakazi wa Ngorongoro wamesema hawajaridhika na maamuzi hayo na kwamba watakata rufaa.

Maelezo ya upande wa  serikali katika utetezi wa tuhuma hizo, yanabainisha kwamba serikali ina haki ya kuichukua ardhi hiyo na kwamba haikutumia nguvu wala uvunjifu wowote wa haki za binadamu wakati wa kuendesha zoezi hilo.