Jumatatu , 22nd Mei , 2017

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, limetolea ufafanuzi malalamiko yaliyotolewa na ndugu za kijana aliyeuliwa na jeshi hilo kwa tuhuma za ujambazi wiki moja iliyopita akidaiwa kujaribu kumpora askari silaha.

Kamishna Simon Sirro

Kamanda wa jeshi hilo Kamishna Simon Sirro amesisitiza kuwa uamuzi wa jeshi hilo ulikuwa sahihi kulingana na mazingira ya tukio na kuwataka ndugu wa marehemu huyo wakatembelee eneo la tukio kusikia wananchi wanasema nini kuhusiana na kitendo cha kijana huyo ambaye aliuawa na polisi baada ya wenzake kukimbia kusiko julikana.

Amesema katika eneo la tukio palikuwa gari la kubebea fedha lililokuwa likisambaza fedha katika mashine za ATM za CRDB kiasi cha Tsh. 320, 000,00 ambapo mtuhumiwa huyo kwa kushirikiana na wenzake alidaiwa kutaka kufanya tukio la uvamizi katika gari hilo, kabla ya askari kumuwahi na kumuua.

Tangu kutokea kwa tukio hilo, ndugu wa marehemu huyo wamegoma kuchukua mwili wake kwa ajili ya maziko wakidai kuwa ndugu yao ambaye pia alikuwa ni mwanafunzi wa UDSM hakuwa muhalifu, huku wakitaka jeshi hilo liombe radhi kwa kudai kuwa ndugu yao alikuwa mhalifu.

Katika hatua nyingine, jeshi hilo limefanikiwa kuua watuhumiwa wanne wa ujambazi 4 katika tukio la hivi karibuni huko maeneo ya mtaa wa Livingstone na Agrey Kariakoo ambapo risasi 65 pikipiki 2 na SMG zikikamatwa na polisi katika tukio hilo.

Kamishna Sirro amefafanua kuwa moja kati ya watuhumiwa hao amewahi kuwaua waendesha bodaboda wapatao 4 katika matukio tofauti jijini humo, ambapo katika tukio hilo raia wanne nao walijeruhiwa na majambazi hao waliokuwa wakifyatua risasi ovyo wakati wakikabiliana na polisi.

Aidha kamanda Sirro amewataka wananchi kuchukuwa tahadhari kubwa pindi wanaposikia kishindo kikubwa ama mlipuko na kuacha kukimbilia eneo la tukio kwani raia waliojeruhiwa ni kutokana na kujazana eneo la tukio bila kuchukua tahadhari.