Jumanne , 17th Jan , 2017

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako amekabidhi hundi ya shilingi 704, 627,856 kwa Halmashauri ya Kaliua ambayo imekuwa ya kwanza kati ya 10 zilizofanya vizuri katika utekelezaji wa mpango wa 'lipa kulingana na matokeo'

Prof. Joyce Ndalichako 

Katika mwaka wa pili wa utekelezaji wa program hiyo ambayo iko chini ya Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (2015/2016), zaidi ya shilingi bilioni 22 zimetolewa kama motisha kwa halmashauri 179 kulingana na jinsi zilivyokidhi vigezo.

Halmashauri zilizoongoza na kiasi cha pesa kwenye mabano ni kama ifuatavyo. Kaliua (704, 627,856), Geita (657,954,115),  Bunda (538,189,807), Rorya (419,338,115), Nzega (415,222,770), Ngara (384,769,590), Itilima (364,387,825), Kongwa (363,652,691) na Chato 336,207,850)

 

Halmashauri zote 10 zilizofanya vizuri zimepewa fedha hizo baada ya kufanya vizuri zaidi kwenye maeneo mbalimbali ya malengo ikiwa ni pamoja na uandaaji mzuri wa takwimu za shule zao, urekebishaji wa ikama ya walimu kwa kuwatawanya ndani ya halmashauri kwa kuzingatia mahitaji na utawanywaji na taarifa za matumizi ya fedha za ruzuku na uendeshaji wa shule kwa usahihi na wakati.

Kwa upande wake Mkurugezi wa Halmashauri ya Kaliua, Bw. John Pima, amesema fedha walizopatiwa na serikali wanazielekeza katika utekelezaji na uboreshaji wa elimu katika halmashauri hiyo na kuongeza zaidi kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi.

Kwa upande wake Waziri Ndalichako amewataka viongozi wote wanaosimamia masuala ya elimu kufanyakazi kwa weledi ili kuleta tija katika sekta ya elimu ikiwa ni pamoja na kuinua kiwango cha ubora wa elimu nchini.