Jumapili , 15th Jan , 2017

Mkoa wa Kagera umetakata katika matokeo ya mtihani wa upimaji wa kitaifa wa darasa la nne kwa kukamata nafasi ya kwanza kitaifa licha ya mkoa huo kukumbwa na janga la tetemeko la ardhi mwezi Septemba mwaka 2016.

Wanafunzi katika moja ya shule za msingi mkoani Kagera

Ufaulu katika mkoa huo ni asilimia 98.83 ambapo jumla ya wanafunzi 48,334 wamefaulu kati ya wanafunzi 48,907 waliofanya mtihani, ikifuatiwa na mikoa ya Kilimanjaro na Geita.

Katika matokeo ya mtihani huo uliofanyika mwezi Novemba mwaka jana (Miezi miwili baada ya tetemeko la ardhi) Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba pia ambayo pia iko ndani ya mkoa huo imeongoza katika halmashauri zote nchini.

Waliofaulu katika manispaa ya Bukoba ni wanafunzi 2,927 kati ya wanafunzi 2,936, ufaulu ukiwa ni asilimia 99.69 ikifuatiwa na Mji Makambako, na Tanga Mjini kama inavyoonekana katika majedwali yafuatayo.

Taarifa iliyotolewa leo na Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA) kupitia kwa Katibu Mtendaji wake, Dkt. Charles Msonde, amesema jumla ya wanafunzi 950,167 kati ya wanafunzi 1,017,713 sawa na asilimia 93.36 waliofanya upimaji huo wameweza kupata alama zenye madaraja ya ufaulu wa A, B, C na D.

Amesema wanafunzi 67,547 sawa na asilimia 6.64 wamepata alama za daraja la E lenye ufaulu usioridhisha.

Takwimu za matokeo zinaonesha kuwa wanafunzi wamefanya vizuri zaidi katika somo la Stadi za Kazi, Haiba Na Michezo, ambapo asilimia 94.67 wamefaulu, huku wakifanya vibaya zaidi katika somo la English Language lenye ufaulu wa asilimia 72.51.

Katika wanafunzi 10 bora kitaifa, wanafunzi 8 ni wasichana wakiongozwa na Loi Martin Kitundu kutoka Fountain Of Joy, huku wanafunzi wawili pekee wakiwa ni wavulana.

Baraza hilo pia limeyafuta matokeo ya wanafunzi 58 waliobainika kufanya udanganyifu