Jumatano , 11th Jan , 2017

Rais wa Tanzania Dkt. John Magufuli amewataka watanzania kuwapuuza  watu wanaoendesha siasa alizozitaja kupitwa na wakati kwa kutumia baadhi ya vyombo vya habari kutangaza kuwa Tanzania inakabiliwa na njaa badala ya kuwahamasisha watu kufanya kazi.

Rais Dkt. John Pombe Magufuli akihutubia wananchi wa Bariadi kabla ya kufungua rasmi barabara ya Bariadi-Lamadi, katika mkoa wa Simiyu

Rais Magufuli ameyasema katika siku yake ya kwanza ya ziara ya siku mbili mkoani Simiyu wakati akizungumza na wananchi katika uwanja wa Shule ya Msingi Somanda mara baada ya kuweka jiwe la Msingi katika  Hospitali ya Mkoa wa Simiyu na kufungua barabara ya Lamadi hadi Bariadi yenye urefu wa kilomita 71.8 iliyogharimu zaidi ya shilingi Bilioni 90.

Amesema kumekuwepo na baadhi ya wanasiasa na wafanyabiasha ambao wamekuwa wakiwahamisisha wananchi na kutumia baadhi ya vyombo vya habari kutangaza baa la njaa wakati wanasiasa hao hao ndio waliopitisha Bungeni kutaka nchi iuze chakula nje ya nchi na sasa hao hao wanatangaza baa la njaa.

 

Rais Dkt. John Pombe Magufuli akiweka jiwe la ufunguzi wa barabara ya Bariadi-Lamadi yenye kilometa 71.8 wengine katika picha ni Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Antony Mtaka, Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira na Muungano Luhaga Mpina, Waziri wa Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, Mwenyekiti wa CCM Simiyu Titus Kamani na Mbunge wa Bariadi Andrew Chenge. Januari 11,2017

'' Baadhi ya wanasisa walizungumza Bungeni kutaka wananchi waruhusiwe kuuza chakula nje ya nchi kwa kuwa kuna chakula cha kutosha leo hii hao hao wanatumia baadhi ya vyombo vya habari kutanga baa la njaa''  

Akizungumzia gharama za  ujenzi wa Hospitali ya mkoa wa Simiyu, Rais Magufuli ameutaka uongozi wa mkoa wa Simiyu, Wizara ya Ujenzi na Wakala wa majengo nchini TBA kukaa na kurejea gharama za ujenzi wa Hospitali hiyo wa Shilingi Bilioni 46 kuwa hauendani na hali halisi ya aina ya jengo linalotakiwa kujengwa.Rais Magufuli ametoa Shilingi bilioni 10 ili kukamilisha ujenzi wa hospitali hiyo. 

''Haiwezekani  majengo ya ghorofa ishirini lijengwe kwa shilingi Bilioni Kumi wakati jengo la ghorofa moja moja lijengwe kwa gharama ya shilingi Bilioni 46''

Rais Magufuli pia ameutaka uongozi wa mkoa wa Simiyu kuendelea na ujenzi wa mradi wa tenki la maji katika mlima Ngasamo ili wananchi wa mkoa wa Simiyu ikiwemo wilaya ya Bariadi kupata huduma ya maji badala ya kukwama kutokana na mwekezaji mmoja kutaka kuchimba madini ya Nikeli katika mlima huo.

Amesema haiwezekani wananchi zaidi ya milioni moja wakose maji kutokana na mwekezaji mmoja ni kukosa muelekeo na kumkosea Mwenyezi Mungu kitu kisichokubalika hivyo Waziri wa Nishati na Madini afute leseni ya mwekezaji huyo ili wananchi wa Simiyu wapate huduma ya maji.

Rais Magufuli amewataka wananchi wa Mkoa wa Simiyu na Watanzania kwa ujumla kutumia mvua chache zinazonyesha kulima mazao yanayostahamili ukame kama vile Mtama,viazi na Uwele ili kuweza kujikimu kwa chakula badala ya kutegemea chakula cha msaada kutoka Serikali.

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akipiga ngoma za asili pamoja na kikundi cha Ngoma za asili Baseki cha Bariadi mkoani Simiyu mara baada ya kuwasili mkoani humo kwa ajili ya ufunguzi wa barabara ya Bariadi-Lamadi.