Jumanne , 25th Jul , 2017

Rais John Magufguli, leo Julai 25, amewaongoza watanzania kwa ujumla, ikiwa pamoja na wananchi wa Singida  waliohudhuria uzinduzi wa barabara ya Manyoni, kuwakumbuka mashujaa wa taifa hili waliopambana katika vita mbalimbali ikiwemo vita ya Kagera.

Dkt. Magufuli aliwataka watu waliohudhuria mkutano huo wa hadhara kusimama kwa dakika moja ili kutoa heshima kwa mashujaa hao kwakuwa leo ni siku ya mashujaa ambayo huadhimishwa kila ifikapo Julai 25.

Kupitia hadhara hiyo Magufuli amevipongeza vikosi vyote vya majeshi ya ulinzi na usalama nchini kwa kazi kubwa wanayofanya, kuilinda nchi na kuifanya kuwa tulivu kiasi cha kuwavutia watu wengine kukimbilia kujiunga na vikosi vya jeshi.

Katika hatua nyingine Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ) limeadhimisha Siku ya Mashujaa kwa kutoa huduma za afya, kuchangia damu na kufanya usafi wa mazingira katika maeneo mbalimbali nchini katika kuwakumbuka na kuwaenzi waliopoteza maisha wakishiriki vita mbalimbali kutetea nchi yao.

Akizungumza na vyombo vya Habari katika viwanja vya Mnazi Mmoja leo Jijini Dar es Salaam, ambako maadhimisho hayo yamefanyika kimkoa, Mkuu wa Majeshi nchini Jenerali Venance Mabeyo amesema, "huduma za jamii zilizotolewa hii leo zinalenga kusogeza jeshi hilo karibu zaidi na wananchi wake sambamba na kuhakikisha mahitaji muhimu ya kiafya hususani upatikanaji wa damu salama ni uhakika".