Jumapili , 15th Jan , 2017

Halmashauri ya Jiji la Arusha imeokoa zaidi ya shilingi  milioni 364 zilizokuwa zitumike kwa ajili ya kuwapa wakandarasi  kwa ajili ya kujenga madarasa badala yake kamati za shule kupewa jukumu la kusimamia ujenzi huo badala ya mkandarasi

Meya wa Jiji la Arusha - Calist Lazaro

Hayo yamebainishwa na Meya wa Halmashauri ya Jiji la Arusha Kalist Lazaro ambapo amesema halmashauri yake imekaa chini na kuona kuliko fedha hizo wapewe wakandasi ili wajenge madarasa ni bora fedha  za ujenzi wa madarasa zipelekwe katika kamati za shule pamoja na bodi za shule ili wasimamie ujenzi huo.

Amesema  sasa hivi halmashauri imetoa shilingi bilioni moja laki nne kwa ajili ya ujenzi wa madarasa 56 ya shule za msingi na fedha zote zilishapelekwa  katika kamati za shule  ili waweze kusimamia ujenzi  mpaka ukamilike.

 Kalisti amesema zamani walikuwa wanatumia wakandarasi  kutangaza tenda kwa ajili ya kujenga madarasa ya shule za  msingi  lakini tangu waanze kujenga madarasa kupitia kamati za shule na siyo wakandarasi wameokoa milioni 364 ambazo wangetumia wakandarasi zote zingeingia katika mfuko wa mkandarasi

Aidha amesema hadi sasa wameshaandikisha wanafunzi wa darasa la kwaza zaidi ya 12, 000 tofauti na mwaka uliopita 2016 ambapo watoto  9600 waliandikishwa kuingia darasa la kwanza na bado wanaendelea kuandikisha hadi mwezi Machi.

Amesema  kutokana na kuwepo na watoto wengi  waliojiandikisha kumekuwa na upungufu wa madarasa  hivyo halmashauri imejenga madarasa 56 kwa ajili ya watoto hao wapya na kukarabati madarasa manne ya shule ya msingi  ambayo yatasaidia  kumaliza tatizo Hilo.