Alhamisi , 29th Oct , 2020

Dr. Hussein Alli Mwinyi, sasa ndiye Rais mteule wa Serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar, baada ya kuwa ametangazwa na Tume ya Uchaguzi
Zanzibar  kuwa amepata kura 380,402 sawa na asilimia 76.27.

Rais Mteule wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dkt Hussein Mwinyi.

Dkt Mwinyi anakuwa Rais wa nane wa taifa hilo tangu Mapinduzi Matukufu
ya 1964, katika hotuba yake ya mwanzo mapema leo baada ya kuwa Rais
mteule amewashukuru Wanzanzibar wote kwa busara zao na uvumilivu zaidi
akiwataka kuja pamoja kulijenga taifa lao na kuziweka tofauti zao
pembeni.

''Niwashukuru zaidi kwa kunipigia kura za kutosheleza kutangazwa na tume
kuwa Rais Mteule wa Zanzibar, ni imani kubwa kwangu na niwahakikishie
nimeipokea imani hii kwa uzito mkubwa, kwa kuwa imani huzaa imani nami
nitawalipa imani hii kwa utumishi uliotukuka'' -
Dkt Hussein Mwinyi.

Mwinyi ameongeza kuwa'' Aidha nitumie fursa hii kuwapongeza wagombea
wenzangu wote tulioshiriki uchaguzi huu, nikiri kuwa nimejifunza mengi
kutoka kwenu, nitatumia yale mazuri yenu mliyoshauri na mliyo ya ahidi
maana lengo letu ni kuijenga Zanzibar, Zanzibar ni kubwa na muhimu
kuliko tofauti zetu''.