Ijumaa , 21st Oct , 2016

Hatima ya wa uwepo wa Umoja wa Mataifa nchini Burundi utategemea kwa kiasi kikubwa uamuzi utakaofanywa na serikali ya Burundi.

Rais wa Burundi Pierre Nkurunzinza.

 

Umoja wa Mataifa umesema hadi sasa mashirika yake yanayohudumu nchini Burundi bado yanaendelea ikiwa ni pamoja na ofisi ya haki za binadamu.

Hivi karibuni serikali ya Burundi ilitangaza kukataa uhusiano wa aina yoyote na ofisi ya haki za binadamu na kutangaza kutowatambua wachunguzi huru watatu waliotumwa na baraza la haki za binadamu kwenda kutathmini hali ya haki za binadamu nchini humo na kisha kuwasilisha ripoti yao kwenye baraza hilo.

Akizungumza na waandishi wa habari Alhamisi mjini New York, msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric amesisitiza kuwa hadi sasa serikali ya Burundi haijatoa uamuzi wa mwisho na kwamba majadiliano yanaendelea.