Jumapili , 20th Aug , 2017

Chama cha Alliance for Democratic Change ADC kimeadhimisha miaka mitano tangu kuanzishwa kwake huku kikiwataka wanasiasa nchini kuwa wakweli na kuendelea kudumisha amani badala ya kutoa kauli na ahadi ambazo zina mwonekano wa kutaka kuleta mpasuko.

Mwenyekiti wa Taifa wa ADC ambaye pia ni Waziri wa Kilimo wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhe. Hamad Rashid Mohamed, ametoa rai hiyo leo jijini Dar es Salaam ambapo amesema kauli za uchochezi zenye kuweza kulewa mpasuko ndani ya chama chake hazikubaliki.

Kauli hiyo Mhe. Rashidi  imedhaniwa kuwa huenda ikawa inamlenga Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad ambaye mara kadhaa amenukuliwa akiahidi kushika wadhifa wa Rais wa Zanzibar.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa ADC Bw. Doyo Hassan Doyo, amevitaka vyama vingine vya upinzani kujenga tabia ya maridhiano pamoja na kusameheana, kama njia ya kumaliza migogoro inayoendelea ndani ya vyama hivyo, kama ambavyo ADC imefanya hivi karibuni kwa kuwasamehe wanachama wake ambao walifukuzwa uanachama miaka michache iliyopita.