Jumatano , 18th Jan , 2017

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo pamoja na mashahidi wenzake wanne wanatarajia kutoa ushahidi katika kesi inayomkabili Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema pamoja na na Mkewe Neema Lema, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, Februari 3, 2017

Godbless Lema (Kushoto) na Mkewe Neema

Kwa mujibu wa Wakili wa Serikali Alice Mtenga amesema licha ya Gambo pamoja na wenzake wanne kutoa ushahidi wao Februari 3 mwaka huu, pia mashahidi hao watakuwa na vielelezo vitatu vitakavyotolewa mahakamani hapo.

Mtenga amesema hayo mbele ya Hakimu, Nestory Barro wakati akiwasomea maelezo ya awali washtakiwa hao ambao ni mume na mke.

Amesema mashahidi watano watatoa ushahidi wao ambao ni Mkuu wa Mkoa Arusha Mrisho Gambo , Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Arusha(RCO) ,George Katabazi, (ASP) Damasi Massawe, mhusika kutoka kampuni ya simu ya Vodacom pamoja na mtaalam wa picha.

Pia amevitaja vielelezo watakavyovitoa katika kesi hiyo kuwa ni nakala ya taarifa za mawasiliano ya simu kutoka kampuni ya Vodacom, Simu ya mshitakiwa ambaye ni ya mke wa Lema ,Neema Lema pamoja na taarifa ya uchunguzi kutoka kitengo kinachoshughulikia masuala ya kiuchunguzi (Forensic Bureau).

Mrisho Gambo Mkuu wa Mkoa wa Arusha

Baada ya kuwasomea maelezo hayo ya awali, washtakiwa hao kwa pamoja walikiri kuwa ni wakazi wa Arusha na Lema ni Mbunge wa Arusha Mjini ila walikataa kusambaza ujumbe huo wa kumtukana Gambo wala tarehe ya kukamatwa kwao.

Naye Hakimu Barro ameahirisha kesi hiyo hadi Februari 3 mwaka huu, ambapo Gambo atafika mahakamani hapo kutoa ushahidi wake ili kuithbitishia mahakama jinsi aliyojisikia vibaya, baada ya kutukanwa na Lema pamoja na Mke wake Neema.