Alhamisi , 25th Aug , 2016

Baraza la Taifa la uwezeshaji wananchi kiuchumi nchini (NEEC) limewatahadharisha wananchi juu ya uwepo wa taasisi au watu binafsi ambao wanawadangaya kuwa mpango wa milioni hamsini katika kila kijiji fedha zimetoka na watoe fedha ili kuzipata.

Katibu Mtendaji Baraza la Taifa la Uwezeshaji wananchi kiuchumi Bi.Bengi Issa (Kushoto) akifafanua jambo kwa waandishi wa habari

Akizungumza katika kipindi cha SUPAMIX kinachorushwa na East Africa Radio, Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) Bengi Issa amesema serikali bado inaendelea na mchakato wa fedha zilizoahidiwa na Rais Dkt. John Magufuli haujakamilika na ukikamilika wananchi watajulishwa.

“ Serikali bado inaendelea na utaratibu wa mpango huu na utakapo kamilika watataarifiwa” Amesema Bengi.

Aidha Bengi ametoa onyo kwa watu binafsi na vikundi ambavyo vinadanganya wananchi wachangie fedha ili kupata fedha hizo watachukuliwa hatua kali za kisheria.

Ikumbukwe kuwa wakati wa uchaguzi wa mwaka jana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliahidi kutoa milioni 50 kila kijiji ili wananchi waweze kunufaika kupitia fedha hizo kwa kufanyia miradi ya maendeleo.