Jumamosi , 23rd Jan , 2021

Mkuu wa wilaya Shinyanga, Jasinta Mboneko, ameuagiza uongozi wa kampuni ya ulinzi ya Suma JKT, kuwachukulia hatua kali za nidhamu walinzi waliohusika kwenye tukio la kumpiga mwananchi Daudi Lefi, aliyefika katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa huo kumuhudumia mgonjwa.

Mkuu wa wilaya Shinyanga, Jasinta Mboneko

Agizo hilo amelitoa hii leo Januari 23, 2021, alipofika hospitalini hapo akiwa na kamati yake ya ulinzi na usalama na kufanya kikao cha ndani na uongozi wa hospitali hiyo na kueleza kuwa hospitali siyo sehemu ya kufanya fujo kwani wananchi wanahitaji huduma.

Jana Januari 22, 2021, katika mitandao ya kijamii ilisambaa video ikionesha walinzi wakimshambulia, mwanaume mmoja aliyejulikana kwa jina la Daudi Lefi, aliyekuwa akitoka kwa ajili ya kutafuta dawa za mgonjwa ambaye ni mama yake, na ndipo walinzi hao walianza kumpiga kwa madai ya kwamba muda wa kuona wagonjwa umekwisha.

Imeelezwa kuwa wakati kijana huyo akishushiwa kipigo na walinzi hao, mdogo wake, Lydia Lefi, alisikika akiwataka waache kumpiga ndugu yake kwa kuwa walikuwa wanakwenda kuchukua dawa.