Jumatano , 11th Jan , 2017

Mkuu  wa  Wilaya ya Arusha Gabriel  Dangalo, amewaagiza wataalamu wa mifugo na kilimo katika  wilaya zote za mkoa wa Arusha, kuhakikisha wanafanya sensa ya kutambua idadi ya mifugo na kuivalisha hereni.

Ng'ombe

Dangalo ametoa kauli hiyo kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo kwenye  hafla ya uzinduzi wa mradi wa kuboresha ng’ombe wa maziwa ADGG, uliowahusisha  wafugaji kutoka halmashauri ya Arusha na jiji la Arusha iliyofanyika mkoani hapa.

Amesema maelekezo ya mkoa ni kuhakikisha ng’ombe wote waliopo kwenye wilaya, mkoani hapa, wanaingizwa kwenye mpango wa utambuzi kwa kuvalishwa hereni, chini ya mradi wa kuboresha mradi wa ng’ombe za maziwa wa  ADGG.

Gabriel Daqarro - Mkuu wa Wilaya ya Arusha

Mratibu wa mradi huo Dk. Eliaman  Lyatuu amesema suala la uwekeji hereni za kitaifa kwa ng’ombe wa maziwa kwa ajili ya utambuzi ni mpango mzuri ambao unafanyika kwa nchi mbalimbali duniani na tayari halmashauri ya Arusha na jiji la Arusha, wameshavalisha ng’ombe wa maziwa zaidi ya 300 .

Ameongeza kuwa mpango huo umepokelewa vizuri na wafugaji na utawasaidia kutambua ng’ombe wao hata pale watakapokuwa wanahamisha mifugo kutoka eneo moja kwenda eneo lingine, pia ng’ombe anapopotea ama kuibiwa inakuwa rahisi kumtambua.