Jumatano , 21st Jun , 2017

Baraza la vijana CHADEMA (BAVICHA) limedai kwamba Baraza hilo litampongeza Rais John Magufuli endapo vigogo wote waliohusika katika sakata la hilo watafikishwa kwenye vyombo vya dola.

Mwenyekiti wa BAVICHA, Patrobas Katambi

Akiongea na vyombo mbalimbali vya habari leo jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Baraza la vijana Chadema (BAVICHA), Patrobas Katambi amesema kuwa wanapenda kuona ufisadi ukishugulikiwa kikamilifu akitolea mfano hatua zilizochukuliwa katika sakata la akaunti ya Tegeta ESCROW, IPTL na mchanga wa madini Makinikia.

Bavicha wamesema kuwa vita ya ufisadi itakuwa na tija endapo wahusika wote walio husika katika kuingiza taifa kwenye mikataba mibovu watachukuliwa hatua, nakumtaka rais kutowafumbia macho hasa wale waliopo ndani ya chama cha CCM kwani bila kufanya hivyo bado ufisadi utalisumbua taifa.

Pamoja na hayo BAVICHA wamelaani kitendo cha kuwekwa ndani kwa masaa 48 Meya wa Ubungo, Mhe. Boniface Jacob, na kutangaza kumfungulia mashtaka mkuu wa wilaya ya Ubungo ndugu Kisare Makori na kutaja kitendo hicho kama nimatumizi mabaya ya madaraka.

Meya wa Ubungo, Boniphace Jacob

Bwana Katambi amesema kosa analotuhumiwa Jacob limekuwa likifanywa mara kadhaa na viongozi wa CCM kufanya siasa za chama kwenye majengo ya Serikali.

“Si kweli kwamba meya alikuwa anafanya siasa alitembelewa na viongozi wengine wa Chadema akawa anawaonyesha mazingira yake ya kazi, ghafla likaja agizo akamatwe, tunaomba tabia hii ikome na safari hii tutachukua hatua,”amesema Katambi.