Jumatano , 20th Jan , 2021

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani Wankyo Nyigesa amethibitisha kutokea kwa tukio la kujinyonga la askari wa Jeshi la Polisi Yusuph Said ambalo limetokea katika eneo la Miembe saba B, kata ya Kongowe Wilayani Kibaha.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani Wankyo Nyigesa

Akizungumza na waandishi wa habari Kamanda Wankyo amesema tukio hilo lilitokea Januari 18 majira ya saa 12 jioni na kutaja kuwa Askari Yusuph alikua akitumikia kituo c na alikua akiishi maeneo ya Picha ya ndege lakini siku ya tukio alienda Kongowe eneo ambalo anaendelea na ujenzi na ndipo alipokutwa amejinyonga na kamba.

Askari huyo mwenye umri wa miaka (52) aliyekuwa anafanya kazi katika kituo cha Polisi Wilayani Kibaha Mkoa wa Pwani  namba   6472 amekutwa  amejinyonga hadi kufariki dunia  katika  nyumba yake anayoijenga katika maeneo ya miembe saba.

Kamanda alibainisha kwamba uchunguzi kuhusiana na tukio hilo unaendelea wakati taratibu za kumsafirisha marehemu kwenda kwao Lindi kwa maziko zikiendelea.

Aidha kwa upande wa Msaidizi wa balozi kwenye eneo hilo Imelda Kitosi alisema akiwa nyumbani alipigiwa simu kuwa kuna tukio la mtu kujinyonga ndipo akaenda kushuhudia akiwa na baadhi ya majirani na alipofika alielezwa na wazazi wa watoto waliokuwa na karibu ya eneo hilo kuwa kuna watoto waliokuwa wanacheza kombolela nje ya nyumba hiyo ambao walisema walisikia mtu anajipiga ndani ya nyumba na walipochungulia wakamkuta tayari yupo chini akiwa na kamba shingoni na walikimbia kwenda kutoa taarifa.