Jumamosi , 31st Oct , 2020

Rais wa Burundi Evariste Ndayishimiye amempongeza Rais mteule wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli,  baada ya hapo jana kutangazwa rasmi kuwa ndiye mshindi wa kiti hicho baada ya kupata kura  12,516,252.

Kushoto ni Rais wa Burundi Evariste Ndayishimiye na kulia ni Rais mteule wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Magufuli.

Rais Ndayishimiye ametoa pongezi hizo kupitia ukurasa wake wa Twitter, ambapo pamoja na pongezi hizo, amewapongeza pia Watanzania kwa kuiamua kesho yao ya amani na kwamba wameonesha ukomavu wa demokrasia.

"Kwa niaba ya watu wa Burundi, na kwa niaba yangu mwenyewe, ninatoa pongezi zangu za dhati kwa Rais Magufuli kwa kuchaguliwa tena, ninawapongeza pia Watanzania ambao wameamua maisha yao ya baadaye kwa amani na kuonesha ukomavu wao wa kidemokrasia", ameandika Rais Ndayishimiye.

Katika kinyang'anyiro hicho jumla ya vyama 15 vilisimamisha wagombea urais, na mara baada ya zoezi la upigaji wa kura na uhesabuji wa kura kukamilika, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), ilimtangaza Magufuli kuwa ndiye mshindi wa kiti hicho na kumshinda mshindani wake Tundu Lissu wa CHADEMA aliyepata kura 1,933,271.