Ijumaa , 27th Nov , 2020

Aliyekuwa mbunge wa jimbo la Mbeya Mjini kupitia CHADEMA, Joseph Mbilinyi maarufu kama Sugu, amesema kuwa kwa sasa hawezi kutoa maoni yoyote juu ya kipi kifanyike kwa wanachama 19  wa chama hicho walioamua kwenda kula kiapo cha ubunge bila ridhaa ya chama.

Kuahoto ni Joseph Mbilinyi maarufu kama Sugu na kulia ni Halima Mdee na Ester Bulaya.

Sugu ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na EATV&EA Radio Digital, na kusema kuwa maelekezo yaliyotolewa na katibu mkuu wa chama hicho Jonh Mnyika, ndiyo ya msingi na kwamba yeye mara baada ya kikao cha kamati kuu kumalizika atatoa maoni yake.

"Mengineyo yatafuata mara baada ya vikao vya kamati kuu kumalizika, mimi siyo msemaji na maoni yangu nitayatoa baada ya kamati kuu kwa sababu na mimi ni mjumbe wa kamati kuu kwahiyo kwa nafasi yangu siwezi kutoa maoni yangu kwa sababu itakuwa siyo fair", amesema Sugu.

Kikao cha Kamati Kuu ya CHADEMA kinakaa leo Novemba 27, 2020, kwa lengo la kuwahoji wabunge hao akiwemo Halima Mdee na wenzake 18, waliokula kiapo cha ubunge ili kujua ni kwanini waliamua kufanya hivyo na baada ya hapo, kamati hiyo itatoa maamuzi dhidi ya wanachama hao.