Jumapili , 27th Sep , 2020

Mgombea Mwenza wa Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi, (CCM), Mama Samia Suluhu amesema katika miaka mitano ijayo chama hicho kitahakikisha kinamaliza changamoto ya maji katika mkoa wa Dodoma na kutekeleza miradi mikubwa ya maji.

Mgombea Mwenza wa Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi, (CCM), Mama Samia Suluhu.

Akizungumza hii leo Septemba 27,2020  katika  muendelezo wa kampeni zake zilizofanyika katika wilaya ya Kongwa amesema kuwa serikali  inafahamu kwamba mkoa huo unakabiliwa na uhaba wa maji  ambapo pia ameahidi kuendeleza utoaji wa Elimu bila malipo.

''Tunajua kuna shida ya maji na tuakuja kuleta maji, tunajua changamoto za uhaba wa maji ziko maeneo mengi ndani ya Dodoma, lakini ndani ya Mpwapwa lakini serikali ndani ya miaka mitano ijayo inakuja kutekeleza miradi mikubwa ya maji'' amesema Samia Suluhu.

''Tunakwenda kuendelea na lile la kusomesha watoto wetu wa kitanzania elimu bila malipo,mzigo huu umebebwa na serikali kutoka kwa wazazi,sasa wengine waje waseme hapa wanakuja kuleta elimu ya aina gani''ameongeza

Aidha amesema kuwa  kuna  mengi yanayofanyika na yatakayoendelea kufanyika ikiwemo  kufufua Shirika la Ndege  kuongeza bandari nchi nzima,kujenga meli na vivuko,pamoja na  kufufua reli za zamani.