ACT Wazalendo wamkaba koo Magufuli kuhusu Katiba

Sunday , 19th Mar , 2017

Chama cha ACT Wazalendo kimemtaka Rais John Magufuli ashughulikie suala la upatikanaji wa Katiba mpya ya Tanzania ambayo mchakato wake ulikwama tangu mwaka 2014 licha ya kufikia katika hatua ya Katiba Pendekezwa.

Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Msafiri Mtemelwa amesema wao kama chama cha siasa wanamtaka Rais Magufuli  kuendelea na mchakato wa kuwapatia watanzania wanyonge Katiba bora kwa kuanzia pale rasimu ya pili ya Jaji Joseph Sinde Warioba ilipoishia.

"Rais Magufuli aanzie na Rasimu ya Jaji Warioba ambayo ilikuwa inatoa nguvu kwa wananchi kuwawajibisha viongozi wao pale wasipotekeleza wajibu wao kulingana na nafasi walizo nazo". Amesema Mtemelwa.

Mtemelwa ameongeza pia "Wakati nchi yetu ikijiandaa kuwapata wawakilishi wapya katika Bunge la Afrika ya Mashariki, Chama cha ACT Wazalendo, tunamuomba Rais Magufuli na tunamkumbusha umuhimu wa watanzania kuwa na Katiba bora itakayoamua maslahi ya nchi katika mfumo ulio rasmi mbali na matakwa ya mtu mmoja pale atakapokuwa anajisikia kufanya hivyo."

Pia amewaomba wadau mbali ikiwemo viongozi wa dini, na taasisi mbalimbali kuweka mkazo katika suala hilo kwa kuwa Katiba iliyo bora itamnufaisha kila mmoja katika jamii