Jumanne , 2nd Mar , 2021

Katibu Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo, Ado Shaibu, amesema kuwa waliamua kumpendekeza Othman Masoud, awe mrithi wa Maalim Seif, kwa sababu ya misimamo yake na uwezo wake uliojipambanua kuhusu maslahi ya Zanzibar na ni mtu ambaye hakutaka sifa za kisiasa.

Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Othman Masoud

Kauli hiyo ameitoa hii leo Machi 2, 2021, kwenye kipindi cha Supa Breakfast cha East Africa Radio, na kuongeza kuwa mchakato wa kupendekeza jina haukuwa rahisi kwani walihitaji mtu ambaye angeweza kuvaa viatu vya Maalim Seif, na kwamba kati ya wanasiasa wote wa Zanzibar hakuna ambaye ameweza kumtilia shaka Othman Masoud.

"Othman Masoud ukiwachambua wanasiasa wa Zanzibar hakuna hata mmoja ambaye atamtilia mashaka katika misimamo yake juu ya maslahi ya Zanzibar na yeye ameshawahi kuonesha misimamo mikubwa isiyotarajiwa pale maslahi ya Zanzibar yanapotishiwa na wakati akiwa Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar alichukua msimamo wa kuipinga Katiba inayopendekezwa katika vifungu visivyozingatia maslahi ya Zanzibar," ameeleza Ado Shaibu.

Jana Februari Mosi, 2021, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Mwinyi, alimteua Othman Masoud, kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar na ameapishwa hii leo.