Jumanne , 22nd Sep , 2020

Naibu Waziri wa Kilimo, Omary Mgumba, ameweka wazi kuwa kuna fursa pana katika soko la korosho kutokana na nchi nyingi duniani zinahitaji korosho zilizobanguliwa.

Mhe. Mgumba amesema hayo akiwa kwenye mkutano na viongozi waliopewa dhamana ya kusimamia zao la korosho ambapo amesema kwasasa tuna masoko mawili ya korosho ambayo ni India na Vietnam.

"Kwasasa tuna masoko mawili tu India na Vietnam zaidi ya hapo huwezi kuuza kwasababu wengine wanakula korosho zilizobanguliwa lakini kuna fursa pana la soko la korosho, kuna nchi za kiarabu, Ulaya,Marekani, China lakini wote wanahitaji korosho zilizobanguliwa” alisema Omary Mgumba

Aidha Mgumba amesema kuwa uongezwaji wa thamani wa korosho umekuwa wa kiasi cha chini sana huku akizitaja faidi zitokanazo na uongezwaji thamani wa zao hilo nchini kabla ya kusafirisha nje ya nchi ikiwa ni pamoja na kuongeza ajira na kupata bei nzuri ya korosho.

“Uongezwaji wa thamani wa zao la korosho pamoja na bidhaa zingine zitokanazo na korosho una faida nyingi ikiwa ni pamoja na kuongeza ajira kupata bei nzuri ya korosho kupanua wigo wa kodi kuinua uchumi wa nchi na kupata soko la uhakika wa korosho zinazozalishwa hapa nchini” alisema Omary Mgumba