Ijumaa , 25th Sep , 2020

Kutokana na kuwepo kwa taarifa za kwamba baadhi ya vikundi vya wajasiriamali ambao wamepatiwa mikopo ya serikali isiyo na riba kuitumia nje ya utaratibu na kukwama kurejesha fedha hizo, Serikali imesema vikundi hivyo ama wajasiriamali wa aina hiyo ni hatari kwa ukuaji wa uchumi wa nchi.

Picha ya moja ya kikundi cha wajasiriamali

Akitoa taarifa ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendelea katika Halmashauri ya Ilala Mkuu wa Wilaya hiyo Ngw'ilabuzu Ludigija, amesema ameamua kuanza ziara rasmi ili kuvibaini vikundi vyote ambavyo vilipatiwa mikopo hiyo.

"Tangu nimeteuliwa kuwa mkuu wa wilaya hii nimekuwa nikizunguka kukagua miradi mbalimbali ya kimkakati ikiwemo Machinjio ya kisasa vingunguti,ujenzi wa masoko mapya ya kisasa ikiwemo soko la Kisutu sasa leo nataka nizungukie vikundi vyote vilivyopatiwa mikopo ili kubaini vilivyo hai na vilivyokwama pesa vilifanyia nini"amesema Ludigija.

Amesema haiwezekani Watanzania wakalipa kodi na tozo nyingine kutoka kwenye vyanzo vyao michango ambayo ndiyo hurudishwa kwa maendeleo ya wananchi halafu wahusika washindwe kufanya hivyo huku akiwataka wafanyabiashara kufuata masharti na taratibu zilizoko kwenye leseni zao za biashara.

Kufuatia changamoto ya wajasiriamali wengi kukopesheka kwenye taasisi mbalimbali za kifedha Serikali iliagiza Halmashauri zote nchini kutoa mikopo yenye masharti nafuu na isiyo na riba kwa makundi ya vijana asilimia nne  wanawake nne pamoja na asilimia mbili kwa watu wenye ulemavu.