Alhamisi , 29th Sep , 2022

Wawekezaji wa sekta ya utalii kutoka mataifa mbalimbali ulimwenguni wanatarajiwa kukutana jijini Arusha katika Mkutano wa 65 wa Shirika la Utalii Duniani (UNWTO) Kamisheni ya Afrika unaotarajiwa kufanyika Oktoba 5-7, 2022 jijini Arusha.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja akizungumza na Kamati ya kitaifa ya maandalizi ya Mkutano wa 65 wa Shirika la Utalii Duniani (UNWTO)

Maandalizi ya mkutano huo wenye kauli mbiu inayosema “Kuujenga Upya Utalii Stahimilivu wa Afrika kwa Maendeleo Jumuishi ya Kiuchumi na Kijamii” yanafanywa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Akizungumza leo katika kikao cha tatu cha kamati ya kitaifa ya maandalizi ya mkutano huo, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja amesema maandalizi yanaendelea vizuri huku akiwaelekeza wajumbe wa kamati hiyo kuendelea kufanya kazi vizuri ili kufanikisha mkutano huo kwa viwango vya juu.

“Ninaamini timu hii ni timu iliyokamilika hivyo kila mjumbe atumie uwezo wake kufanya kazi vizuri ili tusimuangushe Mheshimiwa Rais,” Mhe.Masanja amesisitiza.