Jumatatu , 8th Aug , 2022

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bi. Jenifa Omolo, amesema kuwa Serikali imeongeza bajeti ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2022/23 kutoka Sh. bilioni 294 hadi Sh. bilioni 954 ili kuwezesha sekta ya kilimo kuwa na tija kwa Taifa.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bi. Jenifa Omolo, akifafanua mipango ya Serikali katika kuboresha sekta ya kilimo na utayari wa Wizara ya Fedha na Mipango kushirikiana kwa karibu na Wizara ya Kilimo kufanikisha utekelezaji wa mipango hiyo, alipotembelea Banda la Wizara hiyo katika Maonesho ya Nanenane yanayofanyika kitaifa Uwanja wa John Mwakangale, jijini Mbeya

Bi. Omolo alisema hayo alipotembelea Banda la Wizara ya Fedha na Mipango pamoja na Taasisi zilizo chini yake katika Maonesho ya Nanenane yanayofanyika Kitaifa katika Uwanja wa John Mwakangale, jijini Mbeya.

Alisema kuwa lengo la kuongeza bajeti ni kuwezesha upatikanaji wa mbegu bora, kuimarisha upatikanaji wa pembejeo, utoaji wa elimu kwa wakulima kupitia kwa maafisa ugani, kujenga skimu za umwagiliaji pamoja na kujenga maeneo ya kuhifadhi mazao.


‘Katika bajeti hii ya 2022/2023 Serikali imewekeza fedha nyingi kuhakikisha kuwa kilimo kinatanuka na watu wanapata ajira kwa kuwa asilimia 70 ya Watanzania wanategemea kilimo ambacho ni uti wa mgongo,’ alisema Bi. Omolo.

Alisema kuwa Serikali  imetenga Sh. bilioni 361 ili kuwezekeza katika skimu za umwagiliaji ili kuwezesha wakulima kuendelea na shughuli za kilimo mwaka mzima bila kutegemea mvua za msimu na kiasi cha Sh. bilioni 14.9 kimetengwa kwa ajili ya mafunzo kupitia kwa maafisa ugani ili wakulima waweze kulima kisasa