Alhamisi , 1st Jul , 2021

Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), amesema fedha zitakazopatikana kwenye tozo ya miamala ya simu na bando za mitandao zitapelekwa kutatua changamoto zililizopo pamoja na kwenye miradi mbalimbali  na si kwa ajili ya kulipa mishahara.

Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb).

Dkt. Nchemba amesema hayo wakati alipokutana na kuzungumza na Chama cha Watoa Huduma wa Simu Tanzania (TAMNOA), nakueleza kwamba Watanzania wengi wameunga mkono kutozwa kodi hiyo kwa kutambua umuhimu wa maendeleo ambayo kukamilika kwake kunahitaji mchango wao.

“Fedha zitakazo patikana kwenye tozo hizo hazitatumika kulipa mishahara wala kugharamia matumizi mengine yoyote ya Serikali bali zitapelekwa moja kwa moja kutatua changamoto za afya, elimu, maji, miundombinu ya barabara, elimu na mingine mingi ikiwemo miradi ya kimkakati kama ujenzi wa reli ya kisasa na Bwawa la kuzalisha umeme la Julius Nyerere,” alisema Dkt. Nchemba.

Pia akitoa msisitizo juu ya kodi hiyo, Dkt. Nchemba amesema, “Kampuni za simu msichukulie makato haya kama kodi nyingine mnazowatoza wateja wenu bali Serikali iliamua kuweka makato haya kwenye miamala ya kuweka muda wa maongezi na kufanya miamala kwa njia ya simu ili kuwafanya Watanzania na watumiaji wengine wa simu kuchangia maendeleo ya nchi” 

Aidha, Dkt. Nchemba alitoa muda wa siku 14 kuanzia tarehe 1 hadi 15 Julai, 2021, kwa watoa huduma wote wa Mitandao ya Simu kurekebisha mifumo yao na kuanza kutoza rasmi makato hayo ili Serikali ianze kukusanya fedha hizo.

Kwa upande wao Chama cha Watoa Huduma za Mitandao ya Simu, waliiomba Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango iwape muda wa kurekebisha mifumo yao itakayotumika kukusanya tozo hizo kwa kuwa zoezi hilo linahitaji muda wa kiufundi.

Akizungumza kwa niaba ya Chama hicho, Mkurugenzi wa Uhusiano wa Kampuni ya Simu ya Vodacom Bi. Roselynn Mworia, alisema kuwa chama chao kimeupokea mpango huo kwa mikono miwili na kuwataka wateja wao kuiunga mkono Serikali kwa kuendelea kutumia huduma za kupiga simu na kufanya miamala ya simu.