Jumapili , 4th Dec , 2022

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango ametoa wito kwa wamiliki wa kampuni na taasisi binafsi nchini kuhamasisha na kuzipatia uzoefu kampuni zinazochipukia (business startups) ili kuongeza wigo wa Sekta Binafsi

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango

Makamu wa Rais amesema hayo wakati wa maadhimisho ya siku ya sekta binafsi 2022 nchini Tanzaniailiofanyika Masaki Jijini Dar es salaam.

Amesema Serikali imedhamiria kufanya kazi na Sekta Binafsi katika miradi mbalimbali ya ubia kama vile ujenzi wa barabara, miradi ya umwagiliaji na uzalishaji wa nishati hivyo ameiagiza Wizara ya Fedha na Mipango kwa kushirikiana na TPSF kukaa pamoja na kuangalia namna ya kuongeza ushiriki wa Sekta hiyo katika miradi ya ubia ili kukabiliana na mwitikio mdogo uliopo.

Pia Makamu wa Rais amesema bado Sekta Binafsi haifanyi vizuri katika kuchangamkia fursa mbalimbali na rasilimali za kimataifa katika kulinda mazingira.

Amewasisitiza wadau wote wa Sekta Binafsi chini ya TPSF kwa kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Rais - Mazingira, Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara, na Ofisi za Ubalozi kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kuchangamkia rasilimali fedha za kulinda mazingira kama vile biashara ya hewa ukaa na Green Climate Fund kuibua miradi ya utunzaji wa mazingira ikiwa pamoja na utengenezaji wa nishati mbadala, viwanda vya kuchakata taka ngumu na miradi mingine ya aina hiyo.