Jumanne , 20th Jul , 2021

Waziri wa Kilimo Mhe. Prof. Adolf Mkenda ametoa rai kwa wafanyabiashara wa mbolea nchini kuuza mbolea mapema badala ya kuhifadhi mbolea wakidhani kuwa bei ya mbolea itapanda.

Waziri wa Kilimo Mhe Prof. Adolf Mkenda akizungumza na waandishi wa habari wakati alipofanya ziara ya kikazi ya siku moja katika bandari ya Dar es salaam leo, 20 Julai 2021 kukagua hali ya upakuaji wa mbolea.

Prof. Mkenda ametoa kauli hiyo akiwa katika ziara yake ya ya kikazi ya siku moja katika bandari ya Dar es Salaam na kusema bei ya mbolea kwenye soko la dunia imepanda kwa kiasi kikubwa, nakusisitiza kuwa Serikali inaendelea na mkakati wa kuhakikisha inadhibiti ongezeko la bei ya mbolea nchini.

“Hivyo natoa rai kwa wafanyabiashara wa mbolea nchini wanaohifadhi mbolea wakidhani bei itapanda, hilo hapana itashuka hivyo ni bora kuiuza mbolea hiyo mapema,” amesema Waziri Mkenda.

Pia Waziri Prof. Mkenda amesema kuwa serikali haina kodi kwenye mbolea ila sehemu pekee ya gharama ilikuwa ni ucheleweshaji wa kushusha mbolea pamoja na bei ya soko la dunia, hivyo tayari wizara yake imezungumza na uongozi wa Bandari ya Dar es Salaam ili mbolea inapowasili bandarini ipewe kipaumbele na kuweza kupakuliwa kwa haraka na kuwafikia wakulima kwa wakati

Aidha Prof. Mkenda ameongeza kuwa ili kutatua changamoto za wafanyabiashara tayari Serikali imeshatoa maelekezo kwa Mamlaka ya Mbolea Tanzania (TFRA) kuanza kutoa vibali vya kuuza mbolea ambayo imeshaingia nchini (Export Permit) badala ya vibali hivyo kutolewa Ofisi ya Waziri wa Kilimo kama ilivyokuwa awali, na vibali hivyo vitatolewa kwa njia ya mtandao (Online) badala yake Ofisi ya Waziri wa Kilimo itakuwa na jukumu la kupewa taarifa ya utekelezaji wa utoaji vibali uliofanywa na TFRA.